Makamu wa Rais Dk. Philip Isdor Mpango, amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa taasisi za dini katika kudumisha hali ya amani na utulivu likiwemo dhehebu la dini la Kanisa la Anglicana ambalo hutoa huduma za Injili na Utume kwa pamoja katika ngazi ya kitaifa pamoja na kuendelea kufanya miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.
Katika hotuba yake iliyosomwa mkoani Singida kwa niaba na Mkuu wa mkoa huo Mheshimiwa Halima Dendego, kupitia harambee ya ukamilishaji wa jengo la Kanisa la Parish ya Mtakatifu Paulo, Dayosisi ya Rift Valley mjini Singida, Makamu wa Rais amesema anatambua kazi kubwa inayofanywa na Kanisa la Anglican Tanzania hasa kwenye eneo la elimu kwa ajili ya kuleta maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja kikanda na Taifa kwa ujumla.
"Taasisi za dini ni muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu kazi hii kubwa inayoendelea kufanywa na taasisi hizi imekuwa ni muhimili na kiungo muhimu kati ya Serikali, wananchi na madhehebu kama hili hapa leo...niwaombe endeleeni na moyo huu huu kwa ajili ya faida ya watu wetu wa sasa na hata katika kizazi kijacho...," alibainisha Dk. Mpango.
Aidha Dk. Mpango alihimiza umuhimu wa kuvumiliana na kuendelea kudumisha hali ya amani ili kuzidi kujenga na kuimarisha utulivu hapa nchini ulioasisiwa na watangulizi wa Taifa hili akiwemo hayati Mwalimu Julius K. Nyerere na Sheikh Amani Abeid Karume.
Katika harambee hiyo kwa niaba ya Makamu wa Rais, Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego, aliwasilisha zaidi ya Sh. Milioni 50/-, zikiwa ni fedha taslimu alizoziwasilisha kwa uongozi wa Kanisa la Anglican Tanzania kwa Askofu wa Dayosisi ya Rift Valley Mchungaji John Lupaa, na akawashukuru wananchi na viongozi wote wa mkoa zikiwemo Halmashauri za Wilaya, Sekretarieti ya mkoa na wakuu wa Wilaya kwa kuunga mkono hadi kufanikisha zoezi hilo.
Mapema akisoma risala Katibu wa Kanisa hilo Baraka Mazengo, alisema kuwa tangu ujenzi wa jengo jipya la Kanisa uanze mwaka 2018 hadi sasa mradi huo umetumia zaidi ya Sh. Milioni 313.3/-, na harambee inalenga kukusanya takribani Sh. Milioni 646/-, kuweza kukamilisha kupauliwa kwa jengo hilo litakalokuwa na uwezo wa kuingiza waumini 1,800 kwa mara moja.
Mazengo alifafanua kuwa Kanisa linatarajia hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka huu mradi huo uwe umekamilika.
Kwa upande wake Askofu wa Dayosisi ya Rift Valley John Lupaa, amemshukuru Mheshimiwa Makamu wa Rais na Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuweza kuwaletea wananchi maendeleo kupitia sekta mbalimba kama vile afya, elimu, kilimo, maji na miundombinu ya barabara.
Kupitia harambee hiyo Askofu Lupaa, aliahidi Serikali kuwa fedha zote zilizopatikana zitatumika kwa uaminifu mkubwa katika mipango iliyokusudiwa kwa ajili ya kukamilisha mradi wa ujenzi wa jengo la Kanisa.
Kwenye harambee hiyo zaidi ya Sh. Milioni 137.3/- zilipatikana zikiwemo fedha taslimu na ahadi, kati ya Sh. Milioni 646/- zilizokusudiwa fedha zilizokusanywa zikiwemo fedha taslimu Sh. Milioni 56.9/- na ahadi Sh. Milioni 80.4/-.
MWISHO.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.