Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego, ametoa muda wa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kutuma timu ya Wataalamu wa Ardhi kwenda katika Kituo cha Makazi ya Wazee wasiojiweza cha SUKAMAHELA kwa ajili ya kupima na kuweka mipaka ya kituo hicho ili kudhibiti wananchi wasivamie eneo hilo na kuanzisha shughuli za kiuchumi ikiwemo mashamba.
Dendego ametoa kauli hiyo leo (8-Aprili-2024) baada ya kutembelea Kituo hicho na kukabidhi zawadi mbalimbali kutoka kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwemo Televisheni, friji, nguo, vyakula kwa ajili ya sikukuu ya EID.
Aidha, amesisistiza kuwa baada ya mwezi mmoja kuisha apatiwe taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo vinginevyo atawachukulia hatua Watendaji ambao hawatatekeleza agizo hilo nia ikiwa ni kuhakikisha Wazee wanaotunzwa kwenye kituo hicho wanakaa na kuhudumiwa vizuri bila ya kubughuziwa na mtu.
“Hawa Wazee wametutumikia sana wametufanya tuwe hapa tulipo hivyo ni lazima tuwaheshimu, tuwalee na Tuwatunze” Alisisitiza DENGEGO.
Kuhusu tatizo la kukosekana kwa huduma ya maji na umeme kwenye kituo hicho ambacho kilianzishwa mwaka 1974 kwa ajili ya kutoa huduma kwa Waathirika kwa ukoma, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka Watendaji wa Shirika la Ugavi wa Umeme - TANESCO – Mkoani Singida na wa Mamlaka ya Maji waende kwenye kituo hicho na kuweka kambi ili huduma hizo muhimu ziweze kupatikana muda wote kwenye kituo hicho.
Amefafanua kuwa siku 14 zinatosha kabisa kuweka huduma za maji na umeme kwenye kituo hicho kama hatua ya kuhakikisha wazee hao wanaishi maisha yenye staha ikilinganishwa na hali ilivyo kwa sasa.
Amesisitiza kuwa kupatikana kwa huduma hizo kutasaidia ulinzi kwa wazee hao pamoja na kuwaepusha na vitendo vya kushambuliwa na wanyama wakali hasa nyakati za usiku.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga, amesisitiza Watumishi wa Serikali wanaofanya kazi kwenye kituo hicho kufanya kazi kwa weledi, bidii na ufanisi katika kuwalinda na kuwatunza Wazee hao ili waishi maisha mazuri na yenye furaha kama watu wengine.
Amesema kuwa Wazee ni hazina na baraka hivyo lazima wahudumiwe ipasavyo na kupatia huduma za msingi kama jamii nyingine.
Mkuu wa Kituo cha Makazi ya Wazee wasiojiweza cha SUKAMAHELA Bi. Kusajo Kafuko, ametaja changamoto mbalimbali zinazokwamisha utoaji wa huduma bora kwa wazee hao ikiwemo kukosekana kwa huduma maji, umeme pamoja na kukosekana kwa mlezi wa kiume.
Ameeleza kuwa anaimani kubwa kuwa ujio wa viongozi hao utasaidia kutatua changamoto hizo ambazo zinakwamisha utoaji wa huduma bora kwa Wazee hao walemavu.
Kituo cha Makazi ya Wazee Wasiojiweza cha SUKAMAHELA wilayani MANYONI kilianzishwa mwaka 1974 kwa ajili ya kutoa huduma za tiba kwa Waathirika wa ugonjwa wa ukoma ambapo kwa sasa kinahudumia wazee kutoka Mikoa ya SINGIDA na DODOMA.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.