MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, ametoa onyo kwa wahudumu wa afya mkoani hapa watakaobainika kutoa lugha chafu kwa wazee wanapokwenda kupata matibabu kwenye vituo vilivyoainisha wakibainika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Alitoa onyo hilo juzi wakati wa maadhimisho ya siku ya wazee duniani yaliyofanyika kimkoa katika Wilaya ya Ikungi mkoani hapa.
Serukamba katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Jerry Muro, alisema serikali itahakikisha hakuna mzee atakayetolewa lugha mbaya na wahudumu wa afya.
Alisema serikali imedhamiria kuondoa kero ya upatikanaji wa dawa kwa wazee ambapo hivi sasa upatikanaji kwa mkoa umeongezeka kutoka asilimia 87 hadi kufikia asilimia 94 mwaka 2021/2022.
Serukamba aliagiza katika vituo vya kutolea huduma za afya vitengwe vyumba na madirisha ya kuhudumia wazee na kutolewe matangazo yenye ujumbe unaosomeka kuwa Mpishe Mzee Ahudumiwe Kwanza'.
Kuhusu vitendo vya ukatili kwa wazee, alisema Mkoa wa Singida hautakubari kuona vitendo hivyo vinajitokeza na kuwataka wananchi kuachana na imani potofu vya kishirikina ambazo zinachochea mauaji ya wazee.
Mkuu wa Mkoa alisema hadi kufikia Juni 2022 Mkoa ulikuwa unawatambua wazee 55,920 ambapo hadi sasa wazee 10,385 ambao ni sawa na asilimia 19 wamepatiwa vitambulisho vya matibabu.
Aliagiza viongozi wakiwamo Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanasimamia wazee wote katika wilaya zao wanapatiwa vitambulisho vya matibabu haraka.
Kuhusu uundwaji wa mabaraza ya wazee, Serukamba alisema hilo ni agizo la serikali hivyo lazima litekelezwe na kwamba kwa sasa yapo mabaraza 637 yaliyoanzishwa mkoani hapa katika ngazi za wilaya.
"Nawaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya hakikisheni mnasimamia ili mabaraza yaliyoanzishwa yanafanya kazi kwa ufanisi kama ambavyo yameanishwa kwenye sera ya wazee ya mwaka 2013," alisema.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.