Serikali ya mkoa wa Singida imewaagiza Maafisa Maendeleo wa Halmashauri Saba za mkoa huo kuhakikisha wanafanya tafiti mbalimbali ambazo zitasaidia wanawake wa mkoa huo ambao wanafikia Milioni Moja kuanzisha miradi ya kiuchumi itakayowasaidia kujikwamua na umaskini ikilinganishwa na hali ilivyo kwa sasa.
Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego ametoa kauli hiyo leo (4-Juni-2024) Mjini Singida wakati azindua Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake la mkoa wa Singida kiuchumi.
Halima Dendego amesema jukwaa hilo linatakiwa kuwa na nguvu kuliko majukwaa yote nchini katika kuweka mipango na mikakati madhubuti ya kuwainua wanawake katika masuala mbalimbali ya kiuchumi na uongozi.
“Watoeini Wanawake kwenye mablanketi ya umaskini wasaidieni wainuke kwenye miradi ya kiuchumi wanayoifanya kwa sababu miradi yao mingi haileti matokeo chanya katika kubadilisha maisha ya wanawake, Amesisitiza Halima Dendego.
Amesema hatapenda kuona Jukwaa hiyo linakuwa legelege na kusisitiza kuwa wanawake wengi lazima wajiunge na jukwaa hilo lenye lengo kubwa la kuwasaidia wanawake kujiimarisha kiuchumi kwa sababu wapo wengi na uwezo wao.
Mkuu huyo wa mkoa wa Singida amesema ili kuona Majukwaa hayo ya wanawake yanafanya kazi bila kulala atakuwa anafanya tathimini ya utendaji kazi kila baada ya miezi Mitatu ili kujua maendeleo yao na kama kuna changamoto zinazokwamisha maendeleo ya majukwaa hayo zitatuliwe haraka.
Halima Dendego pia amewahimiza Wanawake wa mkoa wa Singida kujitokeza kwa wingi bila woga katika kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika hivi karibuni kwa sababu uwezo wa kugombea na kushinda nafasi hizo wanazo kinachotakiwa kujiamini na kuthubutu.
Naye, Katibu Tawala wa mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga amewataka Maafisa Maendeleo ya jamii katika Halmashauri Saba za mkoa wa Singida wanakuwa bega kwa bega na wanawake katika kuwashauri na kuwapatia mbinu mbalimbali za kufanya biashara zenye tija ili kuondokana na umaskini wa kipato.
Dkt. Fatuma amesema biashara nyingi wanazofanya baadhi ya wanawake zinaonekana hazina tija hali ambayo inasababisha baadhi ya biashara zinazoanzishwa kufa kwa sababu hawana elimu ya ujasirimali na fedha ikiwemo namna ya kukopa kwenye Taasisi za Kifedha ambazo hazina riba kubwa.
Kwa upande wake, Katibu wa Jukwaa la Wanawake wa mkoa wa Singida akisoma taarifa ya maendeleo ya Jukwaa hilo ambalo kwa sasa linafanya kazi katika Halmashauri Tatu za Singida, Ikungi na Manispaa ya Singida kwa kuwezeshwa na Shirika la UN WOMEN ameomba Serikali kuendelea kuwasaidia wanawake katika elimu ya ujasiriamali, elimu ya fedha na uongozi ili waweze kufanya vizuri katika kujiinua kiuchumi katika biashara.
Nao, Wakuu wa Wilaya za Singida na Ikungi wamemwahidi Mkuu wa mkoa wa Singida kuwa watasimamia kikamilifu maagiza yake katika kuwasaidia wanawake wa Wilaya zao kuwa bora katika masuala ya kiuchumi ikilinganishwa na hali ilivyo sasa.
Mkuu wa Wilaya ya Singida Godwin Gondwe, akitoa neno la shukrani kwaniaba ya Mkuu wa Mkoa huo kwa wanachama wa Jukwaa la kuwezesha wanawake kiuchumi la mkoa wa Singida.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.