Halmashauri za Mkoa wa Singida ambazo zinapata fedha za miradi ya TASAF zimetakiwa kuiendeleza miradi hiyo kwa kuzifanyia matengenezo na kuiongezea thamani ili iweze kuongeza mapato ya wanufaika na Serikali kwa ujumla.
Miradi hiyo ni kama malambo, Mabwawa na Barabara za kijamii.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge alipotembelea Miradi inayotekelezwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF katika Wilaya ya Iramba mkoani hapo ambapo alitoa maagizo ya kuendelezwa kwa miradi hiyo kupitia Halmashauri husika ili iweze kuwa na manufaa zaidi kwa wanufaika.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge akizungumza na Wanufaika wa Miradi inayotekelezwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF katika Wilaya ya Iramba mkoani Singida Mei 26, 2022
Aidha akijibu maombi ya wananchi na wanufaika wa Mradi wa bwawa wilayani Iramba ambao waliomba Serikali kusaidia kuongeza kina na upana wa bwawa hilo, RC Mahenge amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba isaidie matengenezo hayo huku akiwataka kununua vifaranga vya samaki vitakavyofugwa katika bwawa hilo ili liongeze kipato kwao na Serikali kwa ujumla.
Dk. Mahenge ameagiza Maafisa kilimo na mifugo kuhakikisha wanasimamia bwawa hilo ili liweze kuzalisha samaki na liweze kutumika katika Kilimo cha Umwagiliaji wa Mboga mboga na matunda katika eneo hilo.
Katika hatua nyinge RC Mahenge akikagua Ujenzi wa Barabara ya kijamii iliyojengwa na wananchi katika Kijiji cha Misigiri kilichopo kata ya Kiomboi akatumia muda huo kuwaagiza Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini TARURA kuongeza kasi katika uwekaji wa madaraja madogo na makubwa katika barabara hiyo ili ziweze kupitika kwa nyakati zote.
Akimalizia ziara yake katika Kijiji cha new Kiomboi RC Mahenge amewataka wanufaika wa TASAF kutumia fedha wanazopata kwa malengo yaliopo ikiwa ni pamoja na kuanzisha miradi midogo midogo itakayosaidia kuendeleza maisha yao huku akiwataka Maafisa wa TASAF ngazi zote kuongeza juhudi za kuelimisha wananchi kuhusiana na mifumo mbalimbali ya mradi ili kupunguza malalamiko ya wananchi.
Katika taarifa yake DC wa Iramba Suleimani Mwenda amesema kwamba TASAF Wilayani hapo inatekelezwa katika vijiji 51 ikiwemo miradi ya uhaulishaji wa fedha, miradi ya muda mfupi kwa walengwa, kuweka akiba na kukuza uchumi wa Kaya kupitia vikundi pamoja na mradi wa Timiza malengo kwa wasichana balehe na wanawake vijana.
DC Suleimani amesema Halmashauri ya Iramba umepokea kiasi cha Sh. Bilioni 1.184 kwa ajili ya kuandaa Mpango wa manunuzi wa vifaa vya ajira za muda kwa walengwa na Mpango wa kunusuru Kaya maskini, malipo ya ruzuku ya uhaulishaji wa fedha kwa Kaya za walengwa na ruzuku ya ajira .
Aidha, DC huyo amebainisha kwamba vijiji 45 vinatekeleza miradi ya uchimbaji wa malambo wakati vijiji vitano vikitekeleza miradi ya uchimbaji wa Barabara za jamii na Kijiji kimoja kikitekeleza mradi wa Matenga Maji.
Awali akitoa taarifa Mratibu wa TASAF Mkoa Patric Kasango amesema Mkoa umepokea jumla ya Tsh. Bilioni 10 kwa ajili ya miradi mbalimbali iliyopo katika Wilaya za Iramba Ikungi Mkalama Manyoni na Singida ambapo Bilioni 6 kati ya fedha hizo zinatumika kama ruzuku katika masharti ya elimu na Afya.
Baadhi ya Wanufaika wa Miradi inayotekelezwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF waliojitokeza wakati wa ziara ya Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge Wilaya ya Iramba mkoani Singida
RC Mahenge akikagua moja ya Ujenzi wa Barabara ya kijamii iliyojengwa na wananchi katika Kijiji cha Misigiri kilichopo kata ya Kiomboi Wilaya ya Iramba mkoani Singida
Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleimani Mwenda (mwenye suti nyeusi) akisisiza jambo kwa watendaji juu ya usimamizi na utekelezaji wa miradi hiyo wilayani Iramba
Mwisho
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.