Serikali ya Mkoa wa Singida imeendelea kuhimiza uwekezaji katika sekta mbalimbali kama njia madhubuti ya kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, amewataka wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo mkoani humo, akisisitiza kuwa Singida ina mazingira bora, salama na rafiki kwa uwekezaji wa aina zote.
Mhe. Dendego amesema kuwa Mkoa wa Singida uko tayari kwa mapinduzi ya kiuchumi kupitia ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na sekta binafsi huku asisitiza kuwa Serikali inatoa kipaumbele kwa uwekezaji katika sekta za nishati safi, miundombinu, viwanda, kilimo, biashara na huduma, kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.
Aidha, alibainisha kuwa uwekezaji katika nishati safi na salama ni sehemu ya ajenda ya maendeleo endelevu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameweka mkazo mkubwa katika kuhakikisha huduma za msingi zinafika kwa wananchi kwa ufanisi mkubwa, huku mazingira yakihifadhiwa na gharama za maisha zikishuka
Mkuu wa Mkoa pia amepongeza kampuni ya Puma Energy kwa kuendelea kuwekeza nchini, akisema kuwa uwepo wao katika Mkoa wa Singida ni ushahidi kuwa sekta binafsi inaamini katika fursa na mazingira ya biashara yaliyopo nchini.
"Uwekezaji kama huu si tu kwamba unaongeza huduma kwa wananchi, bali pia unaongeza ajira kwa vijana wetu, unachochea mzunguko wa fedha katika jamii, na hatimaye unaleta ustawi wa kiuchumi katika ngazi ya kaya na Mkoa kwa ujumla,” ameongeza.
Kauli hizi amezitoa leo, tarehe 17 Septemba 2025, wakati wa uzinduzi rasmi wa kituo kipya cha mafuta cha Puma Energy kilichopo katika Kata ya Majengo, Manispaa ya Singida, ambapo alikuwa mgeni rasmi. Katika uzinduzi huo, Mhe. Dendego aliwahimiza wananchi na viongozi wa Serikali kuendelea kuwa sehemu ya mazingira mazuri ya uwekezaji kwa kutoa ushirikiano wa karibu kwa wawekezaji wote.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.