Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe Halima Dendego amewaomba wanawake kujiandikisha katika daftari la wapiga kura kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 na kugombea nafasi za uongozi ili wanawake kuwa na nafasi ya kutoa maamuzi pale yanapojadiliwa maswala mbalimbali ya maendeleo.
Hayo yamesemwa hii leo tarehe 16 Octoba, 2024 katika maadhimisho ya kimataifa ya mwanamke wa kijijini yalioanzishwa kwa mara ya kwanza na baraza kuu la umoja wa mataifa mwaka 2007 kupitia azimio maalumu la kutambua jukumu na mchango wa wanawake wa Vijijini katika kuimarisha maendeleo ya Kilimo maendeleo ya vijiji kuboresha usalama wa chakula na kutokomeza umasikini ambayo yamefanyika ukumbi wa shule ya sekondari Ikungi.
Mkuu wa Mkoa amesema kuwa nafasi hizi za uongozi zimewekwa ili wanawake wapaze sauti katika yale ambayo yamekuwa ni kero na yanakwamisha maendeleo ya wanawake kiuchumi na nyanja zingine zote.
"Singida hususani Wilaya ya Ikungi tumeshaanza kuzikataa changamoto za wanawake tunasema tutakapolima tupewe nafasi ya maamuzi kipi kiuzwe na kipi kibaki kwa ajili ya chakula" amesema mkuu wa Mkoa
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Thomas Apson ameongeza na kusema kuwa ipo haja pia wanawake kuwaheshimu waume zao ili kuondokana na migogoro ya mara kwa mara inayojitokeza na kupeleke mifarakano katika familia.
"Nimejifunza hilo kwenye mikutano yangu ya kusikiliza kero za wananchi inapofika saa 12 wanawake wanawahi nyumbani kuwapikia waume zao huu ni Utamaduni mzuri tusiige tamaduni mbaya" ameongeza Mkuu wa Wilaya.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ndg. Richard Rwehumbiza akisoma taarifa mbele ya Mgeni Rasmi kuwa maadhimisho haya hufanyika kila mwaka ili kuelimisha jamii kuhusu jitihada mbali mbali zinazofanyika na serikali na asasi mbalimbali kukuza uchumi na mshikamano wa wanawake nchini na duniani kote.
Naye Afisa Maendeleo ya jamii Bi Haika Massawe mara baada ya maada mbalimbali kujadiliwa juu ya mwanamke wa kijijini ametaja baadhi ya maazimio ambayo kwa kushirikiana na wanawake wa Wilaya ya Ikungi yatatekelezwa kubwa ikiwa ni pamoja na utoaji kwa wakati mikopo ya asilimia 10 za halmashauri na kufatilia utendaji wao wa kazi ili kurejesha mikopo hiyo kwa wakati na mengine ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi kutatua changamoto zao kama kugombea nafasi za uongozi na kujumuika katika kutoa maamuzi.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.