“MPANGO wa kuweka mabango ya anuani za makazi na postikodi usifanywe kisiasa bali ufuate taratibu na sheria zilizowekwa”.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi wakati akifungua mafunzo ya utekelezaji wa mfumo wa anuani za makazi na postikodi kwa watendaji wa mamlaka za Serikali za mitaa mkoani Singida Novemba 5, 2019 yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
” Suala ili naomba lisifanywe kisiasa lifuate sheria na taratibu zilizopo kwani katika maeneo mengine lilichelewa kufanyika kutokana na wanasiasa kutaka majina yao yawekwe kwenye vibao vya mitaa” alisema Nchimbi.
Alisema mpango huu wa kitaifa ni muhimu sana kwani unasaidia wakati wa matukio ya dharura kama moto, sambamba na yale ya kuwafuata wagonjwa katika maeneo yao.
Alitaja faida nyingine kuwa utaweka vizuri mipango miji katika maeneo wanayoishi wananchi, utapunguza migogoro ya ardhi, na utasaidia katika utambuzi wa watu wanapoishi na kuwezesha kupata huduma
za kijamii kwa urahisi.
Dkt. Nchimbi alitumia nafasi hiyo kuwaomba wataalamu wa mkoa wa Singida ambao wamepata mafunzo hayo kwenda kufanya kazi hiyo kwa bidii na weledi huku wakiweka maslahi ya Taifa mbele.
Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Kati, Antonio Manyanda alisema TCRA imekuwa ikitekeleza majukumu yake katika mradi huo kama ilivyoelekezwa katika sera ya Taifa ya Posta ya mwaka 2003 ambayo inalenga kuboresha maisha ya watanzania kwa kupambana na umaskini.
Alisema mpango huo ulianza katika jiji la Arusha ambapo baadhi ya kata ziliwekewa miundombinu ya anuani kama sehemu ya mfano (pilot) na baada ya hapo uliendelea katika jiji la Dodoma ambapo ushahidi wa miundombinu umeonekana.
Kwa habari picha zaidi tembelea: singidars.blogspot.com
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.