Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi leo amekagua miradi ya uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia na Kufundishia katika shule nne za Msingi na sekondari, kama sehemu ya kumbukumbu ya Hayati baba wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Katika ziara yake Dkt Nchimbi ametumia muda mwingi kuwafundisha uzalendo kwa taifa, wanafunzi wa shule za Sekondari Ilongero na Mtinko pamoja na shule za Msingi Mtinko na Mwakichenche zote za Halmashauri ya Wilaya ya Singida.
Dkt Nchimbi amesema, wanafunzi hao watamuenzi mwalimu Nyerere na kudumisha uzalendo endapo watasoma kwa bidii ili taifa lipate wataalamu wa kutosha katika Nyanja mbalimbali watakaoweza kusaidia kukuza uchumi wa Tanzania.
“Mchango wa baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwa taifa letu ni mkubwa sana kwakuwa licha ya kutupatia uhuru pia ametukomboa katika umasikini, ujinga na maradhi, hivyo basi nawaasa muipende sana elimu ili na nyinyi muweze kuwa sehemu ya kulisaidia taifa”, ameeleza Dkt Nchimbi.
Ameongeza kuwa katika kuboresha elimu serikali ya awamu ya tano imetoa zaidi ya shilingi bilioni 1 Mkoani Singida kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kidato cha tano na sita pamoja na kujenga miundombinu ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwa kipindi cha mwaka 2017/2018.
“Tunapomkumbuka Mwalimu Nyerere leo tuthamini mchango wa serikali yetu unaofanya kwa ajili ya kuboresha sekta mbalimbali, mfano katika sekta ya elimu shilingi 1,052, 200,000 zilizotolewa nimethibitisha zimefanya kazi nzuri, kazi kwenu walimu kufundisha kwa bidii na wanafunzi kukazana katika kusoma kwakuwa mazingira yameboreshwa sana”, amesisitiza Dkt Nchimbi.
Aidha Dkt Nchimbi amewapongeza wakuu wa shule na kamati za shule hizo kwa kuchagua mafundi wazawa ambao wametumia gharama nafuu na kujenga miradi hiyo kwa kiwango kizuri, huku akisisitiza wananchi wasijicheleweshee maendeleo kwa kungoja wataalamu kutoka nje ya nchi wakati mtanzania anaweza kufanya jambo hilo kwa ubora ule ule.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida Rashidi Mandoa amesema serikali kuu kupitia program ya lipa kutokana na matokeo imetoa fedha hizo kwa ajili ya shule tatu za Sekondari na mbili za Msingi ili kuinua ubora wa elimu Wilayani hapo.
Mandoa amesema kupitia miradi hiyo inayotekelezwa katika sekondari za Mtinko, Ilongero na Mwanamwema Shein pamoja na shule za Msingi za Mtinko na Mwakichenche, wananchi wameongeza imani na matumaini makubwa kwa serikali yao.
Kwa Upande wake Kiongozi wa Wanafunzi wa Sekondari ya Ilongero Daudi William Kihanga amesema nafasi waliyonayo katika kumuenzi baba wa Taifa ni kusoma kwa bidii kwakuwa wana imani kuwa kila mwalimu anapenda mwanafunzi asome kwa bidii vivyo hivyo wakisoma kwa bidii watakuwa wanamuenzi baba wa Taifa.
Kihanga ameishukuru serikali kwa kuboresha miundombinu ya kujifunzia kwakuwa inawapa wanafunzi hamasa ya kusoma kwa bidii bila kikwazo chochote.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.