Ushirikishwaji mdogo wa Viongozi wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri katika utekelezaji wa miradi ya TASAF kunasababisha miradi hiyo kutokamilika kwa wakati na kushindwa kufikia malengo yalikusudiwa.
Waratibu wa TASAF katika ngazi za Wilaya hawatoi taarifa kwa viongozi wao na kwa Wakurugenzi wa Halmashauri badala yake wanatuma taarifa moja kwa moja kwa waratibu wa kitaifa jambo ambalo limekuwa likiongeza changamoto za kiusimamizi.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge alipohudhuria mafunzo ya mifumo mbalimbali ya uendeshaji miradi ya TASAF yaliyofanyika katika Hotel ya KBH iliyopo mjini hapo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge akizungumza na Viongozi wa Sekretarieti ya Mkoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri (hawapo pichani) waliohudhuria mafunzo ya mifumo mbalimbali ya uendeshaji miradi ya TASAF.
RC Mahenge amebainisha kwamba katika miradi hiyo kuna fedha zinazotolewa kwa ajili ya ufuatiliaji lakini viongozi hawawezeshwi jambo ambalo limekuwa likisababisha miradi kutopata usimamizi unao stahili.
“Ipo miradi ya kijamii kama mabwawa au malambo ambapo kulihitaji kuongezewa nguvu kidogo na Halmashauri kwa kuwa baadaye watachukua ushuru na ajira kwa watu hao zingeongezeka na wangehitimu mapema" alisema RC Mahenge.
Serikali inatoa fedha nyingi katika miradi ya TASAF ambazo kama wakiachiwa waratibu peke yao kuna uwezekano mkubwa wa malengo kutofikiwa hivyo niwaombe wakuu wa Wilaya msaidie kusimamia ili wananchi waweze kunufaika.
Akimalizia hotuba yake Mkuu wa Mkoa amewataka waratibu kuendelea kutoa elimu kwa Wananchi kuhusiana na uendeshaji wa Miradi hiyo kwa kuwa jamiii imekuwa na maswali mengi hasa katika ajira za muda na namna ya ulipaji wa fedha zao.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida Yagi Kiaratu ameipongeza Serikali kwa kuongeza idadi za wanufaika katika miradi hiyo huku akibainisha uwepo wa changamoto kadhaa za kimfumo zikiwemo baadhi ya wanufaika kukosa sifa kwa sababu ya kuwa viongozi na kuomba jambo hilo liweze kuangalia vizuri.
Mafunzo yakiendelea
Katika Mafunzo hayo yaliwahusisha wenyeviti wa Halmashauri ambao kwa nyakati tofauti nao walionesha baadhi ya changamoto katika maeneo na kuomba TASAF makao makuu kuangalia namna ya kuzitatua.
Awali akitoa taarifa ya Mradi wa TASAF awamu ya pili Kaimu Meneja wa malipo kwa walengwa na uhaulishaji fedha Kitaifa Msangi Tsetonga amebainisha kwamba Mradi una gharama ya Dola za Kimarekani 883.31 sawa na Trilioni 2.03 ambayo ni sawa na asilimia 0.5 na walengwa ni Milioni 1.45 ambao utambuzi ulifanyika katika Vijiji zaidi ya 6000.
Bwana Msangi amesema tathmini inaonesha kwamba kuna Kaya zenye uwezo wa kufanya kazi zipatazo 979,918 sawa na asilimia 67 wakati familia zenye uwezo wa kufanya kazi lakini hazina watoto ni 190,988 sawa na asilimia 13.2 ki Taifa.
Mratibu huyo akabainisha kwamba jumla ya Kaya 179,821 sawa na asilimia 12.4 ni Kaya za wazee walemavu na wagonjwa wa muda mrefu na hazina watoto.
Mafunzo hayo yalihudhuriwa na wakuu wa Wilaya wenyeviti wa Halmashauri Wakurugenzi wakuu wa Idara na waratibu wa Mradi.
MATUKIO KATIKA PICHA
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida Yagi Kiaratu (kushoto) pamoja na Wenyeviti wa Halmashauri za Wilaya wakishiriki Mafunzo hayo.
Sehemu ya Sekretarieti ya Mkoa wa Singida wakishiriki Mafunzo hayo.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.