Vijana mkoani Singida wametakiwa kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali ili kutumia fursa ya uwepo wa maeneo ya mashamba yaliyotengwa kila Halmashauri kwa ajili ya Kilimo cha pamoja (block farming) ili kuongeza kipato na ajira.
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Singida wakati wa ziara yake katika Wilaya ya Mkalama na kuwataka vijana kujiunga katika vikundi ambavyo vitaweza kupewa mashamba makubwa kwa ajili ya Kilimo cha vitunguu na alizeti.
"Kila Halmashauri zimetenga maeneo ya mashamba kwa ajili ya Kilimo cha pamoja hivyo fursa kwa vijana kujiunga katika vikundi na kuvisajili ili Halmashauri zao ziweze kuwakopesha mitaji kupitia asilimia 10 na wawekeze katika kilimo cha alizeti au Vitunguu." Alisema Dk. Mahenge
Ameagiza vijana ambao wanajishughulisha na kilimo kuhakikisha kinafanywa ki Biashara ili kuongeza tija ambapo amesema kilimo cha pamoja kitasaidia kupata mikopo sehemu mbalimbali na urahisi wa kupata huduma za ugani kwa pamoja.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge (kushoto) akimpongeza Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Mkalama Lameck Tungi, kwa kuwekeza katika kilimo cha vitunguu
Hata hivyo RC Mahenge akatumia nafasi hiyo kwa kumpongeza Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wa Wilaya kwa kuwekeza katika kilimo cha vitunguu na kwa hatua aliyoichukua ya kuwasaidia Vijana wengine katika matumizi ya maji ya Umwagiliaji kwa kutumia miundombinu aliyoitengeneza kwa gharama ya zaidi ya Milioni 40.
Aidha Rc Mahenge ameendelea kumpongeza Mwenyekiti huyo kwa kutoa ajira kwa vijana zaidi 90 ambao wanasimamia miradi ya shamba la vitunguu na mabwawa ya samaki huku akihamasisha vijana kujiunga katika shughuli za kilimo.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo akizungumza na baadhi ya wananchi wa Kata ya Bumagwa wilayani Mkalama wakati wa ziara hiyo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo amesema wamejipanga kuimarisha vikundi vya vijana kwa kutoa mikopo mikubwa kwa vikundi vichache ili waweze kuwekeza kwa kiasi kikubwa
Hata hivyo DC Kizigo amesema Wilaya hiyo imejipanga katika mwaka huu wa fedha kuvikopesha vikundi kupitia asilimia kumi ambayo kuna mgawanyiko wa asilimia nne kwa vijana, nne kwa wanawake na mbili kwa watu wenye ulemavu lengo likiwa ni kuhakikisha vikundi hivyo vinatoa ajira kwa watu wengine.
Akitolea mfano wa kikundi kilichopo Iguguno DC Kizigo amesema Halmashauri ya Mkalama ilitoa mkopo wa Milioni 25 na kuwapatia Mradi wa kufyatua tofali 6000 kwa ajili ya Ujenzi wa shule jambo ambalo liliwasaidia kutoa ajira kwa watu wengi.
Akizungumza kuhusu vikundi vya vijana kuwekeza katika kilimo DC Kizigo amesema ili vijana waweze kupata faida kupitia kwenye kilimo ni lazima wawe tayari kulima ekari kuanzia tano na kuendelea.
Kwa upande wake Lameck Tungi Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mkalama ambaye ni mkulima wa vitunguu katika shamba lenye ukubwa wa ekari 14 amesema kwa utaalamu uliotumika katika shamba hilo anategemea kuvuna magunia 1200 kwa sababu limekuwa na mchanganyiko wa mvua na umwagiliaji.
Amesema uwekezaji wake katika eneo hilo kumeleta hamasa kwa wakulima wengine ambapo zaidi ya ekari 18 zimelimwa kuzungukia bwawa alilolichimba kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mkalama Lameck Tungi (kulia) ambaye ni mkulima wa vitunguu katika shamba lenye ukubwa wa ekari 14, akizungumza wakati wa ziara katika shamba hilo.
Lameck ametoa wito kwa vijana kushiriki katika kilimo cha pamoja ili kupata urahisi wa huduma za ugani na masoko ambavyo vitaondoa changamoto ya ukosefu wa ajira.
Ziara hiyo ya Mkuu wa Mkoa ililenga kukagua hali ya Kilimo katika eneo hilo, ukaguzi wa Ujenzi wa Kituo cha Afya Bumagwa Ujenzi wa shule ya Nyeri na kuangalia maendeleo ya Ujenzi wa miradi ya maji katika Wilaya hiyo ya Mkalama.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge wakati alipotembelea shamba hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge akishiriki uchimbaji wa msingi kwa ajili ya Ujenzi wa Kituo cha Afya Bumagwa wilaya Mkalama leo Aprili 13, 2022
www.singida.blogspot.go.tz
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.