Wazazi wametakiwa kutumia fursa zilizopo katika Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) ili kuwajengea vijana wao uwezo wa kupata elimu ya ufundi inayowawezesha kujiajiri ambavyo Serikali, kupitia Wizara ya Elimu imeendelea kuongeza bajeti kwa vyuo hivyo, ikiwemo VETA, ili kuhakikisha vijana wanapata ujuzi wa vitendo utakaowasaidia kujitegemea.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhe. Godwin Gondwe, Februari 25,wakati wa uzinduzi wa maonesho ya Chuo cha Ufundi VETA Kanda ya Kati, kuelekea maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) tangu kuanzishwa mwaka 1994.
Katika hotuba yake, Mhe. Gondwe ametoa wito kwa Mamlaka ya VETA Kanda ya Kati kushirikiana na viwanda mbalimbali katika Wilaya ya Singida ili kuwaongezea wanachuo ujuzi wa vitendo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Singida na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Musa Sima, amesema kuwa mpango wa kuwatambua na kuwasimamia vijana walioko mtaani wenye ujuzi wa ufundi binafsi na kuwapatia vyeti rasmi ni hatua muhimu kwa maendeleo yao.
Aidha, amesema kubwa Serikali imewataka wahitimu wa elimu ya juu kujiunga na VETA ili kujipatia ujuzi wa vitendo utakaowawezesha kujiajiri badala ya kutegemea ajira za ofisini pekee.
Akizungumzia kodi ya ukuzaji ujuzi (SDL) inayotozwa kwa waajiri kwa asilimia 6, Mhe. Sima amesisitiza kuwa ni muhimu kuhakikisha fedha hizo zinatumika kuboresha elimu na miundombinu ya VETA nchini.
Naye Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati, Ramadhani Makata, amewahimiza wazazi na vijana kujitokeza kwa wingi kujiunga na vyuo vya VETA kwa lengo la kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kuinua uchumi wao.
"VETA ndiyo mkombozi wa taifa hili. Vijana wanapaswa kuitumia fursa hii kujiandaa kwa maisha bora kupitia elimu ya ufundi stadi," alisisitiza Makata
Maadhimisho hayo yamefanyika katika viwanja vya Bombadia, Mjini Singida.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.