Viongozi mbalimbali Mkoani Singida wamehesabiwa pamoja na familia zao katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linaloendelea kufanyika leo nchi nzima.
Akiongea baada ya kuhesabiwa katika Mtaa wa Utemini ambapo ndipo makazi yake Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba ametoa wito kwa kila mwana Singida kuhakikisha anahesabiwa ili kujua idadi kamili ya watu na Serikali iweze kujipanga kuwahudumia katika kipindi cha miaka kumi ijayo.
Amesema usiku wa kuamkia tarehe 23 Agosti mwaka huu Makarani Mkoa wa Singida walitembelea maeneo ya vituo vya mabasi na kwenye nyumba za wageni ili kuweza kuhesabu watu walikuwamo humo.
RC Serukamba amesema kwamba Mkoa umejipanga kuhakikisha kila mwananchi anahesabiwa ikiwemo maeneo yaliyokuwa na changamoto ya kiutawala baina ya mipaka ya Mkoa na Wilaya ikiwemo Mkoa wa Manyara na Dodoma kwa upande wa Wilaya Nchemba.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Pasikas Muragili amewataka wananchi ambao hawataweza kuhesabiwa siku ya leo kwamba bado kuna siku sita mbele za kuhesabiwa huku akiwakumbusha kuacha taarifa muhimu kwa wakuu wa kaya ikiwemo mawasiliano ya simu pindi wanapotoka kutafuta mahitaji yao ili waweze kuhesabiwa.
Aidha Mhandisi ameweza kuhesabiwa pamoja na familia yake baada ya kutembelea na Karani aliyepangwa katika eneo hilo.
Ameeleza kwamba siku ya jana wakishirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya walifanikiwa kutatua changamoto za baadhi ya Kata ambazo wakiwa na migogoro ya mipaka ya kiutawala hiyo wananchi hao kuridhia kuhesabiwa.
Mwenyekiti wa CCM Juma Kilimba amebainisha kwamba Sensa ni muhimu katika utekelezaji wa Ilani na kwamba kwa kujua idadi ya watu kutasaidia chama kuweka mikakati mbalimbali ya kuwahudumia wananchi.
Aidha Kilimba ameendelea kuwasihi wananchi wa Mkoa huo kuhakikisha wanatumia siku ya leo na ndani ya siku sita zijazo kutoa ushirikiano mkubwa kwa Makarani wa Sensa kuhesabiwa.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.