Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu Mhe. Asina A. Omari amesema kuwa tume inatarajia kupata ushirikiano mkubwa zaidi kutoka kwa wadau mbalimbali walioshiriki kwa kuwafikishia wananchi wa Mkoa wa Singida taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa kuwahamasisha wote wenye sifa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha.
Ameyasema hayo katika mkutano wa tume na wadau wa uchaguzi Mkoani Singida katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Singida uliohudhuriwa na wadau mbalimbali ikiwemo viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, wawakikiahi wa asasi za kiraia, wahariri wa vyombo vya habari, waandishi wa habari, maafisa habari wa mikoa na halmashauri, wawakilishi wa makundi mbalimbali ya vijana, watu wenye ulemavu, wanawake na wazee wa kimila.
"Ni matarajio ya Tume kuwa mtakua mabalozi wazuri wa kusambaza taarifa na kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao ili zoezi hilo lifanyike kwa ufanisi na kwa matokeo makubwa". alisema Mhe. Jaji Asina.
Ameongeza kuwa lengo la mkutano huo ni kuwapa taarifa za uwepo wa zoezi hilo na kuwapitisha katika mifumo ya uandikishaji pamoja na kuona namna zoezi litakavyofanyika vituoni na taarifa za maandalizi ambayo yanajumuisha uhakiki wa vituo vya wapiga kura, uboreshaji wa majaribio, ununuzi wa vifaa na ushirikishwaji wa wadau.
Pia, amewaomba viongozi wa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi kuzingatia sheria ya uchaguzi, kanuni za uboreshaji, maelekezo ya tume na kusimamia miiko na mipaka ya uendeshaji wa zoezi la uboreshaji wa daftari huku akisisistiza kuwa mawakala au viongozi wa vyama vya siasa hawaruhusiwi kuingilia mchakato wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kituoni.
Katika Mkoa wa Singida, tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 216,947 ikiwa ni ongezeko la asilimia 26 ya wapiga kura 848,456 na kuwa na idadi ya wapiga kura 1,065,403 katika mzunguko wa tano wa uboreshaji daftari.
Kaulimbiu ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura 2024/2025 inasema "KUJIANDIKISHA KUWA MPIGA KURA NI MSINGI WA UCHAGUZI BORA".
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.