Timu ya Madaktari bingwa wa Mama Samia ambayo leo imeagwa rasmi Mkoani Singida,imefanikiwa kuwafikia na kuwahudumia wagonjwa 3,242 kupitia kambi ya kliniki tembezi iliyofanyika kwa siku tano katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, Mandewa.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, ameongoza hafla ya kufunga rasmi kambi hiyo leo Mei 9,2025 akisema kuwa amefurahishwa na mafanikio ya kambi hiyo aliyoitaja kuwa ni ya kupongezwa kwa tija kubwa iliyoonekana kwa wananchi waliopata huduma.
"Kwa maana hiyo basi, mimi sina budi kumshukuru Mungu kwa ajili yenu, na kwa kila mmoja aliyechangia katika zoezi hili.Tumewagusa wananchi, tumewagusa wana Singida, na Watanzania wenzetu ambao walitaabika kwa muda mrefu kwa kukosa huduma, lakini kupitia ninyi mmeweza kurudisha faraja na afya katika maisha yao."amesema Daktari Mganga
Pia Dkt. Mganga amewapongeza madaktari wa Mkoa wa Singida kwa kutumia rasilimali zilizopo kuongeza pato la hospitali na huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt.Shilla Mwashiuya, ametoa pongezi kwa madaktari bingwa kwa kazi nzuri tangu walipoanza kambi tarehe 5 Mei akisema kuwa mirejesho kutoka kwa wagonjwa mbali mbali waliopata huduma hizo ni mizuri sana kwani wamefurahibkuoata huduma bora na karibu kabisa na makazi yao hapa Mkoani Singida.
" Wagonjwa waliopata huduma wameridhika na matibabu na kauli nzuri kutoka kwa madaktari. Kupona si dawa tu, bali hata kauli njema inachangia mgonjwa kupata faraja," amesema Dkt.Shilla
Mwenyekiti wa Madaktari Bingwa wa Dr. Samia, Dkt. Amani Malima, amtoa taarifa ya utekelezaji wa kazi hiyo amesema kuwa waliwahudumia wagonjwa 3,242 dhidi ya lengo la 3,000, na kufanikisha upasuaji kwa wagonjwa 82 bila mgonjwa yeyote kuhitaji rufaa.
"Wagonjwa wetu wote tuliowafanyia upasuaji wametoka salama, na hakuna aliyelazimika kupelekwa hospitali nyingine. Hii ni dalili kwamba tumepunguza gharama kwa wananchi na tumevuka malengo yetu," alisema Dkt. Malima.
Aliendelea kusema kuwa kambi hiyo ni ya tatu kwa awamu ya kwanza Kanda ya Kati, baada ya Morogoro na Iringa, na kwamba wataelekea Dodoma na Njombe kwa awamu zinazofuata. Ameushukuru uongozi wa Mkoa wa Singida kwa mapokezi mazuri na ushirikiano uliowezesha zoezi hilo kufanyika kwa mafanikio.
Wananchi nao wameeleza kwa furaha kuridhishwa na huduma walizopata kutoka kwa madaktari bingwa waliowahudumia kwa upendo na juhudi kubwa.
"Madaktari wa Samia wanatoa huduma nzuri sana na wako vizuri. Nimefurahi sana kwa huduma zao na tunaomba awamu nyingine waje kututembelea tena."Mimi nimepata uponyaji mkubwa kwa sababu mwanangu amefanyiwa upasuaji hapa. Nawaomba madaktari hawa waendelee hivyo hivyo na wapande ngazi kwa kazi nzuri wanayoifanya."amesema Amina Mwanga
Kwa mafanikio haya, Mkoa wa Singida umejizatiti kuendelea kushirikiana na timu ya madaktari bingwa ili kuhakikisha huduma bora zinaendelea kuwafikia wananchi wengi zaidi katika awamu zijazo.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.