Wahandisi wa miradi ya maendeleo ikiwemo majengo ya madarasa na vituo vya Afya Mkoani Singida wametakiwa kuwa wabunifu na kutumia utaalamu wao katika kuwashauri viongozi kufanya miradi hiyo kwa awamu ili kukamilika kwa wakati na kuweza kuleta tija kwa muda mfupi.
Hayo yamesemwa leo na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Sahili Geraruma wakati wa kuweka jiwe la Msingi katika mradi wa shule ya Sekondari Kitalaka iliyopo Halmashauri ya Itigi wilayani Manyoni.
Gararuma amesema Wahandisi wanayo nafasi ya kushauri katika ujenzi kulingana na kiasi cha fedha zilizopo ili kujenga majengo machache yanayokamilika kwa muda mfupi na yakatumiwa na wanafunzi kuliko kujenga majengo mengi yasiyoisha kwa wakati uliyopangwa.
Amesema miradi mingi haikamiliki kwa wakati kwa sababu Wahandisi wanashindwa kushauri kulingana na taaluma zao jambo ambalo linachangia miradi hiyo kutokamilika kwa wakati na kujikuta inahitaji muda wa ziada.
"Ukifanya hesabu vizuri utajua kwamba fedha ulizonazo zinaweza kujenga jengo la namna gani au majengo mangapi, unaona una fedha za June majengo matano na unaanza mpango unataka majengo kumi kwa nini usishauri yaanze kujengwa kulingana na fedha iliyopo", aliuliza Geraruma
Amewataka wasimamizi wa majengo hayo kuwa na Mpango kazi ambao utaonesha ni kila kazi na muda wake na itasaidia kujipima wenyewe kama kazi waliojipangia inakamilika kwa wakati.
Aidha akiwa katika kituo cha Afya Mitundu Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru ameagiza viongozi wasimamie misingi na maadili ya kazi zao huku akiwasihi mafundi kukagua vifaa vya ujenzi kabla ya kuvipeleka stoo.
Kiongozi huyu amebainisha kwamba vipo vifaa kadhaa vimepokelewa katika kazi mbalimbali za Ujenzi na kuhifadhiwa stoo wakati ndani yake sivyo vilivyokubaliwa.
Mwisho
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.