Mkuu wa Wilaya ya Singida Godwin Gondwe leo Disemba 05,2024 amemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego katika uzinduzi wa zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya kidijitali kwa wajasiriamali wadogo wadogo mkoani Singida ambao umefanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Singida.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi na wawakilishi mbalimbali akiwemo Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya viwanda na biashara, Maafisa maendeleo ya jamii kutoka ngazi za Mkoa na halmashauri ambao ni waratibu wa dawati la wafanyabiashara ndogo ndogo,Viongozi wa Wafanyabiashara ndogo ndogo(wajasiriamali) na wawakilishi kadhaa wa wafanyabiashara ndogo ndogo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Mkuu wa Wilaya amesema ni wakati sasa wa wajasiriamali kwenda kunufaika na fursa mbali mbali kutokana na kupata vitambulisho hivyo huku akitoa agizo Kwa waratibu wa zoezi hilo wilaya zote kuongeza kasi ya kuandikisha wajasiriamali hao ili wengi waweze kunufaika.
“Shughuli ya uzinduzi na ugawaji wa vitambulisho vya kidigitali kwa ajili ya Wafanyabiashara ndogondogo katika Mkoa wa Singida umetokana na changamoto ya muda mrefu ya kutaka kuwatambua wafanyabiashara ndogondogo nchini kwa idadi yao na umuhimu wa kuweka utaratibu mzuri wa kuwaratibu ili waweze kukua katika shughuli zao za kiuchumi na kijamii Kwa lengo la kuwainua wafanyabiashara hao kiuchumi na kijamii pamoja na utayari wa kuhakikisha kuwa changamoto zao zinapatiwa ufumbuzi na wataalam kwa wakati”. Amesema DC Gondwe.
Awali,Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya viwanda na biashara,Bi.Donatila Vedasto ameainisha makundi ya Wafanyabiashara ndogondogo,
"Wafanyabiashara ndogondogo nchini tunazingatia biashara zote halali zinazofanywa na wafanyabiashara hao ambazo zinatambuliwa na Mamlaka. Aidha, wafanyabiashara ndogondogo wanajumuisha machinga, mama na baba lishe, madereva wa bodaboda na bajaji, wasusi, vinyozi, wakulima wa bustani ndogondogo na wauzaji wa vyakula kama vile matunda na mbogamboga. Kwa ujumla sekta hii inachangia kwa kiwango kikubwa kutoa ajira kwa vijana wanaohitimu katika ngazi mbalimbali za elimu na taaluma hapa nchini”. Alisema Bi.Donatila
Wema Yona mfanyabiashara ambaye amepata kitambulisho siku ya Leo,amesema anategemea kupata fursa nyingi zaidi kupitia vitambulisho hivyo vya wafanyabiashara ndogo ndogo ikiwemo fursa za kupata mikopo ambazo walikua hawazipati ,akisema kuwa sasa watafanya kazi kwa kujiamini zaidi huku akitoa wito kwa wajasiriamali wote kupata vitambulisho hivyo ili kuwa karibu na fursa.
Pia,ameomba ushirikiano wa kutosha kutoka kwa viongozi uendelee ili kuweza kuzitatua changamoto zitakazojitokeza kwa lengo la kukuza uchumi wa wajasiriamali mmoja mmoja na Singida kwa ujumla kwa kuongeza mapato kutokana na kulipa kodi.
Mpaka sasa takribani wajasiriamali 894 wameshasajiliwa na kupata vitambulisho hivyo Mkoani Singida.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.