Wajumbe wa Kamati ya Usalama ya mkoa wa SINGIDA ikiongonzwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Dkt. REHEMA NCHIMBI wametembelea na kukagua maeneo yote yaliyoathirika na mvua kubwa iliyonyesha hivi karibuni na kusababisha nyumba tatu kubomoka pamoja na baadhi ya maeneo kutitia katika Kijiji cha KITOPENI halmashauri ya Wilaya ya Itigi mkoani Singida.
Akizungumza na Wananchi wa Kijiji hicho Dkt. Nchimbi amewaomba wananchi wanaoishi katika maeneo hayo kuwa watulivu pamoja na kuchukua tahadhali katika maeneo hayo na amewaahidi kuwa Serikali itatuma wataalamu wa Jiolojia ili kufanya uchunguzi wa kina kama hatua ya kujua nini hasa kimesababisha tukio hilo litokea.
“Kwa Wananchi wote kwanza tuchukue tahadhali kwa eneo hili, lilivyo tuu katika muundo wake linaonekana kwamba kuna namna ambavyo inatakiwa litazamwe, lipimwe na lipewe tathimini inayofaa ili kutambua kama linafaa kwa makazi ya binadamu au halifai, na kama litaonekana linafaa basi tutaona namna gani tuweze kuwategemeza ili muendeleze makazi yenu, lakini likionekana kwamba halifai kwa makazi basi tutatoa maelekezo mengine”.
Kwasababu Serikali wakati wote kazi yake ni kuhakikisha usalama wa raia na mali zao na ulinzi wa wananchi na Taifa, Wataalam Serikali inao, imewafundisha wataalam hao, imewasomesha wataalam hao, kuna mabingwa wa kuangalia miamba na mielekeo ya namna hii”. Amesema Dkt. Nchimbi.
Aidha, Dkt. Nchimbi amewaagiza viongozi wa vijiji, mtaa na vitongoji kuweka ulinzi wa kutosha ili kuhakikisha watoto kutoathiliwa na maafa hayo na amewataka wananchi wa eneo hilo kutoa ushirikiano pamoja na kutoa taarifa za mapema wakati wowote pindi watakapoona viashiria vyovyote vile vyenye kuleta maafa ili hatua za haraka zichukuliwe.
Nao, Wananchi wa Kijiji cha KITOPENI katika halmashauri ITIGI wilayani manyoni wamesema, wakati mvua kubwa ikinyesha walisikia ngurumo iliyofuatiwa na kishindo kikubwa hali ambayo ilisababisha sehemu ya ardhi hiyo kutitia, nyumba TATU kubomoka na kutokea kwa mashimo hayo marefu pamoja na nyufa katika baadhi ya ardhi.
Hata hivyo, Wananchi hao wameishukuru Serikali kupitia Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Singida ikiongonzwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Dkt. REHEMA NCHIMBI kwa ziara yao yenye tija na malengo ya kuhakikisha suluhisho la maafa hayo sambamba na upatikanaji wa wataalamu hao wa Jiolojia.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya ITIGI wilayani Manyoni Mhe. PIUS LUHENDE amesema kuwa, Katika tukio hilo hakuna vifo wala majeruhi ya watu zaidi ya nyumba na baadhi ya vitu viliyokuwemo ndani ya nyumba hizo kuharibika.
“ Hakuna athari kubwa, hakuna mtu aliye kufa wala kuumia, hasa ni nyumba zilizoanguka na vifaa vilivyokuwemo ndani ya nyumba hizo tumevitoa na na kuvihifadhi kwa majirani. Lakini pia tumewaambia kama mtu anahitaji nyumba, tuna nyumba ya mwalimu haina mtu, shule zimefungwa na madarasa yapo. Lakini wote wamesema wanakaa kwa ndugu zao kwa hiyo hakuna tatizo”. Amesema Mhe. Luhende.
Kwa muujibu wa Wananchi wa KITOPENI wamesema hili ni tukio la kwanza kutokea kwenye kijiji chao cha KITOPENI halmashauri ya Wilaya ya Itigi mkoani hapa.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.