Serikali ya Mkoa wa Singida imewataka wakulima na wafanyabiashara kuendelea kutumia mfumo wa stakabadhi za ghala kwa tija kubwa ili kuwaepusha na walanguzi wa mazao ya biashara na kuimarisha biashara yao.
Akizungumza na Waandishi wa habari, tarehe (6 Septemba, 2024), Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mheshimiwa Halima Dendego, amesema kuwa mfumo huu umeanza kutekelezwa rasmi katika msimu wa 2024/2025 mkoani humo.
Aidha ameeleza kuwa utekelezaji wa mfumo huo unafuatia maagizo yaliyotolewa na serikali kupitia mwongozo wa biashara ya mazao kama dengu, mbaazi, na ufuta, ambao umetolewa chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Tume ya Ushirika, Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala na Soko la Bidhaa kupitia toleo la tatu la mwaka 2024.
Mkuu wa Mkoa pia alibainisha kuwa mwongozo huu mpya unalenga kudhibiti biashara ya mazao na kuwahakikishia wakulima na wafanyabiashara masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi. Kupitia mfumo huu, wakulima watapata bei nzuri kwa mazao yao ikilinganishwa na miaka iliyopita, na hivyo kuongeza mapato yao.
Amefafanua kuwa, bei ya zao la dengu ambayo ilikuwa inauzwa kati ya TZS 900 hadi 1300 kwa kilo katika msimu wa 2023/2024, sasa inauzwa kati ya TZS 1,670 hadi 2,060 kwa kilo katika msimu wa 2024/2025 kupitia mfumo wa stakabadhi za ghala.
Faida nyingine za mfumo huu ni pamoja na ongezeko la mapato kwa halmashauri, udhibiti wa utoroshaji wa mazao, na kutoa uhakika wa takwimu kwa serikali. Mfumo huu pia umewezesha upatikanaji rahisi wa mikopo kwa wakulima na kuongeza masoko ya uhakika ya ndani na nje ya nchi.
Hata hivyo, amesema, ubora wa mazao umeimarika kwa kiasi kikubwa kutokana na mfumo huu ambao unazingatia taratibu na viwango bora vya usafirishaji na uhifadhi wa mazao, pia mfumo wa stakabadhi za ghala umeleta mapinduzi makubwa katika biashara ya mazao mkoani Singida.
Serikali ya Mkoa wa Singida inaendelea kushirikiana na wadau wote muhimu ili kuhakikisha mfumo huu unatekelezwa kikamilifu na kuleta matokeo chanya kwa wakulima na wafanyabiashara. Hii ni hatua muhimu katika kukuza uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla kupitia sekta ya kilimo, ambayo inabaki kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.