Jumla ya Tsh. Milioni 136.1 kati ya Milioni 339.62 zimerejeshwa katika akaunti za Halmashauri ya Wilaya ya Iramba kutoka kwa wadaiwa (Deforters) ikiwa ni fedha zinazotokana na makusanyo ya mapato kupitia mashine (posi) baada ya Mkuu wa Mkoa huo Peter Serukamba kusimamia kidete madeni hayo.
Akiwa katika kikao cha kukutana na wadaiwa hao kilichofanyika leo katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo RC Serukamba aliyeambatana na Kamati ya Mkoa ya ulinzi na usalama aliwataka wadaiwa hao kuwasilisha risiti za malipo benki au fedha taslimu kwa wahasibu waliokuwepo katika ukumbi huo.
Baada ya mahojiano ya muda mrefu kwa kila mdaiwa ilionekana wengi wao walikwisha lipia jana yake lakini risiti zao walikuwa hawajaziwasilisha kwa wahasibu wa Halmashauri hiyo.
Aidha Serukamba amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Michael Matomora kusimamia kikamilifu Idara ya uhasibu ambayo ilionekana kutotekeleza wajibu wao katika kufuatia wadaiwa hao ambapo amewataka wahakikishe kila mwenye mashine ya makusanyo anapeleka fedha Benki kila siku.
Amesema uwepo wa wadaiwa sugu imetokana na wahasibu kutofatilia pindi wanapogawanya mashine za kukusanya fedha na wakati mwingine kutohakiki madeni ya risiti wanazopatiwa na wadaia hao.
Hata hivyo Serukamba ameagiza kupatiwa taarifa za makusanyo kila baada ya siku mbili ionyeshe kiwango cha madeni kilichokusanywa pamoja na makusanyo mapya.
Kwa upande wao wadaiwa wakati wakihojiwa wengi wao waliahidi kulipa fedha hizo zilizobaki katika kipindi cha wiki mbili hadi miezi mitatu ijayo huku wengine wakiishia mikononi mwa Polisi baada ya kutoa taarifa halisi.
Aidha amewataka wasimamizi wa mfumo wa fedha katika Halmashauri hiyo kuhakikisha wanahakiki madeni ndani ya mfumo ambayo yameshalipwa na kuyafuta ili yabaki madeni halisi.
Halmashauri hiyo kwa sasa inadai jumla ya sh. Milioni 203.51 baada ya wadaiwa wengine kulipa madeni yao.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.