Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe.Halima Dendego ameagiza waalimu kuwekeza nguvu ya ziada ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi pamoja na msingi wa kuwawezesha kuendana na mazingira ya mtaani baada ya kuhitimu elimu yao ya Sekondari.
Ameyasema hayo (Novemba 5,2024)alipotembelea Shule ya Sekondari Mitundu na kukagua ukamilishaji wa vyumba viwili vya madarasa katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi.
Akizungumza katika kikao na waalimu wa Shule ya Sekondari Mitundu amesema ni vema waalimu kuongeza nguvu za ziada ili kupunguza ufaulu mbaya kwa wanafunzi kutokana na matokeo yasiyoridhisha ya shule hiyo,akisema ni vema kuzitambua changamoto za wanafunzi na namna ya kuzitatua kupitia semina,na kutiwa moyo na watu waliofanikiwa kama Viongozi ambao watawaona kama mfano kwao ili kuwapa motisha ya kusoma kwa bidii.
"Pamoja na kusoma darasani,wanafunzi wafundushwe stadi mbali mbali za maisha ikiwemo kilimo,usafi,kishiriki katika michezo na mchaka mchaka ili kuchangamsha akili,pia ni vema kupewa adhabu pale inapostahili kwani ni namna ya bora ya malezi bora kwa kuwaandaa kuwa na tabia njema"alisema Dendego.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mitundu,amesema waalimu wa Shule hiyo wameazimia kutumia njia mbali mbali ya kuongeza ufaulu wa wanafunzi ikiwemo kuanza kuweka kambi shuleni kwa madarasa ya mitihani(kidato cha pili na kidato cha nne) kwa kufundishwa muda kwa muda mrefu ma uangalizi wa karibu,pia kwa kujisomea wenyewe alfajiri.
"Kuanzia sasa tumejiandaa kikamilifu kwa ajili ya oparesheni kabambe ya kutokomeza ufaulu wa daraja la nne na daraja ziro,kwa kutumia njia mbali mbali za kibunifu na kuwaweka wanafunzi wetu karibu,itakuwa rahisi kuzitambua changamoto zao kwa urahisi na kuwaweka katika mazingira salama kiakili kwa ustawi wa taaluma zao."alisema mwalimu.
Sambamba na hilo,Mkuu wa Mkoa alihudhurua katika Mkutano wa kusikiliza na kutatua kero mbali mbali za wananchi wa kijiji cha mitundu na kuagiza ufuatiliaji katika utendaji kazi mzuri wa masuala ya huduma za afya,kilimo,matumizi ya stakabadhi ghalani,umeme na maji ya uhakika.
Pia amesisitiza mikopo ya wajasiriamali kutolewa kwa vijana,wanawake na walemavu hususani maeneo ya kijijini kwa lengo la kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja,kaya na kijiji kwa ujumla.Kutokana na mikopo hiyo kuwafikia wanufaika hao vijijini itakuwa chachu kwa maendeleo ya sekta nyingine ikiwemo bara bara,vituo vya afya,umeme na maji kwani mzunguko wa fedha utakua mzuri na kuchochea maendeleo.
"Ni wakati sasa wa wananchi wa kijijini kufikiwa na mikopo ya wajasiriamali kwa wingi kuliko mjini,hivyo ni wajibu wako muhusika kuhakikisha unawabainisha wahitaji wenye vigezo husika ili nao wanufaike na mikopo hiyo ambayo ni mtaji tosha kwao katika safari ya kujikwamua kiuchumi".alisema Mhe.Dendego.
Naye Diwani wa kata hiyo,Bw.Masanja Patrick ametoa shukrani za dhati kwa serikali kutokana na maendeleo makubwa yaliyotokana na utekelezaji wa shuhuli mbali mbali za maendeleo katika eneo hilo ikiwemo ujenzi wa vyumba vipya vya madarasa,upanuaji wa kituo cha afya na kukarabati bara bara zinazounganisha makao makuu ya kata na miradi mingine mipya ambayo bado haijakamilika kwa asilimia mia moja.
John Jackson,mkazi wa Kijiji cha Mitundu akizungumza baada ya Mkutano wa kijiji na Mkuu wa Mkoa amesema wamefurahishwa na ujio wa Mkuu wa Mkoa katika kijiji chao kwani itakua chanzo cha utekelezaji mzuri wa changamoto zote za wakazi wa eneo hilo kupatiwa ufumbuzi.
"Kupitia ziara hii ni wazi kuwa changamoto zetu zinakwenda kutatuliwa kwa kiasi kikubwa,nasi tunafurahi kuona kiongozi wetu ana utayari wa kuja hadi ngazi ya kijiji kwa ajili ya kusikiliza na kutatua changamoto zetu hivyo tuna imani kuwa kuanzia sasa miradi na huduma mbali mbali zitakwenda vizuri kwani ufuatiliaji wake upo katika mikono salama."alisema Bwana Jackson.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.