Zaidi ya Wananchi 16,000 wa Kata ya Msange, tarafa ya Ilongero katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida, watanufaika na mradi wa Kilimo cha umwagiliaji, baada ya Serikali kupitia Wizara ya Kilimo chini ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kuingia mkataba wa ujenzi wa bwawa litakalogharimu zaidi ya Sh. Bilioni 17.705
Mradi huo ni sehemu ya miradi sita katika mkoa wa Singida kati ya 100 nchini kote ambayo Rais aliwaahidi Watazania kujenga mabwawa ya umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa mavuno na uchumi kwa wananchi hususani kwenye mikoa ambayo hutegemea mvua mara moja kwa mwaka.
Mkuu wa mkoa wa Singida Mheshimiwa Halima Dendego, amesema hayo wakati wa makabidhiano ya mradi yaliyofanyika katika kijiji cha Msange kati ya Serikali Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na Mkandarasi aliyeshinda zabauni hiyo Kampuni ya Kagwa General Supplies Limited ya mkoani Singida.
“Nimshukuru sana Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutuletea mradi huu pamoja na mingine mitano kwenye mkoa wetu na hili linadhihirisha ni jinsi gani anatujali sisi watu wa Singida, nchi nzima kuna miradi 100 lakini hapa Singida Rais ametupendelea kwa kutupatia mabwawa sita ya umwagiliaji,” alisema.
Dendego amesema, mradi huo utakuwa mkombozi kwa wananchi wa eneo hilo na kuwataka wautunze ili waweze kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula mbogamboga na yale ya biashara kwa ajili ya kuinua uchumi wao na taifa kwa ujumla.
Amesema pamoja na mradi huo kunufaisha wakulima 3,000 kutokana na ekari 3,500 zilizopo kwenye eneo la mradi lakini zaidi ya wananchi 16,000 watanufaika kupitia shughuli za kilimo na hata uzalishaji wa mazao yatakayopatikana baada ya mavuno na shughuli nyinginezo za mradi.
“Mradi huu unaenda kunufaisha vijiji vinane vyenye zaidi ya watu 16,000 kaya 3,000 mnataka Mungu atupe nini, tunasema umaskini baibai Singida…hatuwezi kuwa na mradi wa bilioni 17 hapa tushindwe kuleta mbegu bora ili tuongeze mavuno yetu naomba sana tuutunze mradi huu…,” alisisitiza RC. Dendego
Awali Mhandisi wa umwagiliaji mkoa wa Singida kutoka Tume ya Taifa ya umwagiliaji Japheth Senyinah, alisema mkataba wa mradi ni wa miaka miwili huku ukitarajiwa kukamilika Julai, 27 mwaka 2027 ukihusisha ujenzi wa bwawa miundombinu ya umwagiliaji nyumba za watumishi wa mradi na gari lililogharimu Sh. Milioni 110, litakalotumiwa na wafanyakazi katika kurahisisha majukumu mbalimbali.
“Licha ya ujenzi wa bwawa mkandarasi atajenga pia barabara za mashambani zenye urefu wa kilomita 9.2 ujenzi wa ofisi ya mradi ujenzi wa nyumba za watumishi watakaosimamia mradi kujenga mfereji mkuu utakaokuwa unasambaza maji mashambani wenye urefu wa mita 1,370 madaraja na mifereji midogo 6,470…,” alibainisha Senyinah.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Msange ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida Eliya Dighah, alisema katika makabidhiano hayo kuwa pamoja na changamoto zinazotolewa na baadhi ya wananchi wasiutakiwa mema mradi huo lakini anaamini Serikali itautatua na kuumaliza kabisa tayari kuanza uzalishaji wa mazao mbalimbali.
Kupitia hadhara hiyo Dighah aliishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kufanikisha mradi huo ambao utakuwa na umuhimu mkubwa na mkombozi kwa wakulima wa vijiji nane vya Kata yake.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa huyo alipata nafasi ya kuhimiza wananchi hao kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotaraji kufanyika mwaka huu ambapo amewahimiza wale wote wenye sifa za kugombea wasisite kuchukuwa fomu na pindi siku ya uchaguzi ikifika wananchi wote kushiriki kwenye uchaguzi wa viongozi waliowaadirifu ikiwepo pasipo kutumia rushwa.
Mkuu wa Mkoa wa Singida (katikati) akishuhudia utiaji saini wa makabidhiano wa mradi huo
Mkurugenzi wa Kampuni ya Kagwa General Supplies Limited ya mkoani Singida Mhandisi Kagwa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo picha) mara baada ya makabidhiano ya mradi huo.
Baadhi ya wakazi wa Kata ya Msange ambapo mradi unatekelezwa wamemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mradi huo.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.