Mkoa wa Singida umeandaa tamasha kubwa litakalo washirikisha wanawake zaidi ya 3,000 kutoka wilaya zote za mkoa huu lililobeba jina la Wanawake na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, akizungumza leo (Oktoba 7, 2024) na waandishi wa habari, amesema tamasha hilo litafanyika Oktoba 10, mwaka huu kwenye viwanja vya Bombadia vilivyopo Manispaa ya Singida.
Amesema Spika wa Bunge mstaafu ambaye pia ni Kamisaa wa Sensa nchini, Anne Makinda, atakuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo ambalo lengo lake ni kuwahamashisha wanawake kushiriki katika uchahuzi wa serikali za mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 27, 2024.
"Serikali yetu bora na sikivu chini ya uongozi wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, imeweka taratibu mbalimbali za kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata taarifa sahihi za uchaguzi na anahamasishwa ili aweze kushiriki katika uchaguzi na hivyo kutimiza haki yao ya kikatiba, hivyo tamasha hili ni moja ya mipango ya mkoa katika kuwafikia wananchi wengi hasa makundi maalum ya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu," amesema Dendego.
Dendego amesema tamasha hilo ni fursa kubwa na ya kipekee kwa wanawake wa Mkoa wa Singida kushiriki pamoja na mama Anne Makinda ambaye ni kiongozi mbobezi ili waweze kupata ladha sahihi ya wanawake na uongozi na matumizi ya takwimu katika kufanya maamuzi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
"Kongamano letu litahusisha wanawake takribani 3,000 kutoka wilaya zote tano za Mkoa wa Singida na kubwa zaidi wanawake hawa vinara wanatoka kwenye ngazi za chini kabisa kwa maana ya vijiji mitaa na kata," amesema Dendego.
Ameongeza kuwa lengo la kuwakutanisha wanawake hao ni kuwahabarisha na kuwahamasisha kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa,uchaguzi ambao unatoa viongozi watakaosimamia maisha yao ya kila siku.
"Pamoja na tamasha hili,bado kuna mikutano mbalimbali inaendelea mabonanza ya michezo yanaendelea na ziara za viongozi nazo zinaendelea, lengo ni kiwafikia wananchi walio wengi na hasa maeneo ya pembezoni na kuwaleta pamoja kwenye jambo hili kubwa katika nchi yetu," amesema Dendego.
Aidha, amesema tamasha hili mbali na kuwaleta pamoja wanawake vinara litaanbatana na taarifa fupi za maendeleo na uzinduzi wa mpango wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na litasindikizwa na burudani kutoka kwa wasanii mahiri.
"Tamasha hili la wanawakenwa Mkoa wa Singida linalobeba kauli mbiu Serikali za Mitaa,Sauti ya wananchi jitokeze kushiriki uchaguzi si la kukosa,atakuwepo msanii Msaga Sumu na singeli Isha Mashauzi na miondoko ya pwani na mwanamama mshereheshaji Angela Bondo," amesema Dendego
"Nawakumbusha wanawake wa Mkoa wa Singida,tamasha hili tumeliandaa pamoja na tushiriki pamoja kuliheshimisha na kujiheshimisha,hivyo mjitokeze kwa wingi sana ili tamasha lipendeze ikiwa ni moja ya safari ya kuwaunganisha wanawake katika mambo muhimu yanayogusa maisha yao," amesema Dendego.
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 Mooa wa Singida unakadiriwa kuwa na watu 2,008,058 na nusu ya hao zaidi ya milioni moja watashiriki kwenye uchaguzi kutokana na kukidhi vigezo.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.