Jamii imetakiwa kuwapa nafasi wanawake katika kumiliki ardhi kwani kufanya hivyo itasaidia kumpa Mwanamke haki na usawa katika Jamii .
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 19.02.2025 na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Halima Dendego wakati akizungumza na Standard Radio katika kipindi cha asubuhi cha Zinduka, kuelekea kilele cha siku ya mwanamke duniani.
Amesema kuwa Jamii ya Mkoani Singida imekuwa na changamoto ya kutokuwapa nafasi wanawake kumiliki mali ikiwemo ardhi ikiamini kwamba mwanamke ni dhaifu na hana uwezo wa kusimamia na kumiliki ardhi.
Kadhalika,Mkuu wa Mkoa Mhe.Halima Dendego amewasisitiza wanawake wajitokeze kushiriki kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba mwaka huu.
Mhe.Dendego amesema kuwa kujitokeza kwa wanawake katika kushiriki kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu kutaleta chachu ya maendeleo na kujisimamia wenyewe katika mambo yao pamoja na kuongeza haki na usawa katika jamii.
Katika hatua nyingine Mhe.Dendego amesema kuwa kwa sasa wanawake wamekuwa ni chachu ya kuleta maendeleo hivyo jamii wakiwemo wazee wa kimila na viongozi mbalimbali wawape haki ya kumiliki ardhi kwani wana uwezo wa kusimamia na kuongoza katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Siku ya Mwanamke duniani huadhimishwa Machi 8, kila mwaka na kwa mwaka huu siku hiyo kitaifa itafanyika Mkoani Arusha, kwa mkoa wa Singida itaadhimishwa tarehe 07.03.2025 katika uwanja wa Bombadia Manispaa ya Singida huku Kauli mbiu mwaka2025 ikiwa 'Haki, usawa na uwezeshaji''.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.