WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua shamba la mfano la korosho lenye ukubwa ekari 12,000 lililopo kijiji cha Misigati, wilayani Manyoni na kusema kuwa ameridhishwa na uamuzi wa wilaya hiyo kuwa na zao mbadala la biashara.
Akizungumza na wananchi na baadhi ya watumishi wa Halmashauri hiyo waliokuwepo eneo hilo Oktoba 4, 2019, Waziri Mkuu alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi kwa kulibeba wazo hilo na kuhakikisha linatimia.
“Nimpongeze Mkuu wa Mkoa kwa kulibeba jambo hili, lakini nikuombe wewe na viongozi wenzako mhamasishe wengine walime zaidi zao hili kwa sababu korosho ni zao kubwa duniani na tena zao hili lina bei nzuri kimataifa,” alisema.
Alisema anatambua kwamba timu ya wataalamu kutoka kituo cha utafiti wa kilimo cha Naliendele, Mtwara imeshawasili Manyoni ili kufanya utafiti wa zao hilo na jinsi linavyoweza kuzaa mara mbili kwa mwaka.
“Kwa kawaida, mkorosho mmoja hutoa kilo 40 za korosho kwa msimu mmoja, kwa hiyo kwa misimu miwili mtapata kilo 80. Ninawasii limeni korosho kwa ajili ya watoto wenu ambao wako darasa la pili au la tatu. Mkulima ukianza kuvuna, utaendelea kuvuna kwa miaka 20 mfululizo na kwa hiyo hao watoto hawatahitaji kulipiwa ada wakiwa chuo kikuu sababu korosho itakuwa inawalipia,” alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wakulima wanaolima zao hilo wilayani Manyoni, waunde Ushirika wao ambao utawasaidia kuagiza dawa kwa pamoja ama kuuza kwa pamoja. Hivyo, amemwagiza Afisa Ushirika wa Wilaya hiyo, Bi. Yusta Philipo ahakikishe anasimamia jambo hilo kuanzia sasa.
Mapema, akitoa taarifa juu ya mradi huo, Meneja wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Kanda ya Kati, Bw. Ray Mtangi alimweleza Waziri Mkuu kwamba mradi wa kilimo cha korosho unajumuisha mashamba makubwa mawili ambapo shamba la Masigati lina ukubwa wa ekari 7,000 na lile la Mikwese lenye ukubwa wa ekari 5,000.
Alisema watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa kitaifa wamekuwa wakifika shambani hapo ili wajifunze mbinu mpya za kuzalisha korosho kwenye maeneo yao. “Wiki mbili zilizopita, Mheshimiwa Spika na madiwani wa Kongwa walipita hapa ili kujifunza zao hili,” alisema.
Pia alisema Halmashuri yao imetenga eneo la ujenzi wa viwanda na kwamba hadi sasa wanazo ekari 50 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kubangua korosho.
Waziri Mkuu alikagua shamba hilo na kujionea hali halisi ya shambani ikoje. Pia alioneshwa mabibo na korosho ambazo zimevunwa kutoka kwenye shamba hilo la mfano, kutoka kwenye mashamba ya wakulima ambao walipanda miche tangu Januari, mwaka jana.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.