Wakazi wa Mkoa wa Singida wametakiwa kujitokeza kwa wingi na kupata chanjo ya Uviko 19 ambazo zinatolewa na wataalamu wa afya katika vituo mbalimbali ili kuwa na mtaji wa kiafya utakaosaidia kuongeza uzalishaji na kuimarisha uchumi wao.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Binilith Mahenge alipokuwa akifungua kikao cha kamati ya Afya ya msingi Mkoa (PHC) kilichofanyika leo katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Dkt. Binilith Mahenge amesema kwamba ili kuleta maendeleo makubwa katika Mkoa wa Singida ni muhimu kulinda afya za watu na kuwaepusha maradhi ili waweze kuwa na nguvu za kuzalisha.
Aidha Mkuu wa mkoa amewataka wataalamu wa afya kuendelea kuwafuata wananchi majumbani na kutoa chanjo kwa hiari kwa kuwa imeonekana kusaidia wananchi ambao kwa sababu moja au nyingine wanashindwa kufika vituo vya kutolea huduma ya chanjo.
Hata hivyo ametoa wito kwa wataalamu wa afya kuendelea kutoa elimu juu uchanjaji iendelee kutolewa kwa wananchi ili kuhamasika na uchanjaji ambapo kwa sasa hakuna dawa ambayo imeshapatikana ya kutibu uviko 19.
Amewataka wananchi kuendelea kunawa na kutumia vitakasa mikono ili kuepuka maambukizi ambayo yanaweza kuathiri maisha yao.
Aidha Dkt. Mahenge amesema kwamba kikao kazi hicho kimelenga kutathmini zoezi la utoaji wa chanjo ya korona mkoani hapo Janssen katika awamu ya kwanza na kuangalia namna ya uendeshaji wa zoezi la pili kwa uharaka zaidi.
Amesema kwasasa mkoa unaendelea na utoaji wa chanjo aina ya sinopham japo mwitikio bado haujawa mzuri hivyo kuwataka wananchi kujitokeza kupata chanjo hizo ili kujiepusha na athari za ugonjwa wa UVIKO 19.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.